Tuesday, November 3, 2009

KITABU CHA MAISHA NA MAFANIKIO......

SEHEMU YA PILI...................

Huwezi kuwa kamili bila mwingine kukamilika

Sisi kama binadamu tunajipenda na hakuna awezaye kulizuia jambo hili. Lakini kujipenda kwa ziada kunaweza kuzuilika kama mtu ataamua. Kujipenda kwa ziada ndiko ambako kunapelekea dunia kuwa kama ilivyo leo kwa upande wa uharibifu. Yale yote ambayo hayakwenda sawa kufuatana na mpango wa Mungu yamesababishwa na uziada wa kujipenda kwa binadamu, Mpango wa Mungu ni kuwa na dunia ambayo haina makovu wala vidonda. Lakini dunia hii tunamoishi imejaa vidonda na makovu zaidi kuliko uzima. Vidonda na makovu haya, kama ambavyo tumesema ni matokeo ya binadamu kujipenda kupita kiasi, kujipenda ambako kunamfanya adhani kwamba yeye anastahili zaidi kuliko mwingine na kumfanya awe pia mvivu wa kufikiri.

Ni binadamu wachache sana ambao wako tayari kukaa chini na kujiuliza kama kweli wana tofauti na wengine. Ni wachache kwa sababu kila mmoja anaamini kwamba ni taofauti na mweingine, iwe ni kwa mwenye mali au asio nayo, iwe ni kwa mwanamke au mwanaume, au kwa msomi au asiyesoma, kila mmoja anaamini kwamba ana tofauti na mwingine. Anashindwa binadamu kujua kwamba, yeye kama binadamu hana tofauti na binadamu mwingine.

Labda tukumbushane kwamba binadamu hawi binadamu kwa sababu ana magari makubwa mia moja au ana nyumba za fahari mji mzima, lakini pia hawi binadamu kwasababu anashinda na kulala na njaa au anatembea makalio yakiwa nje kwa ulitima (Umaskini). Binadamu anakuwa binadamu kwa sababu kuna sifa ambazo hupatikana kwake na kwa mwingine bila kujali huyo mwingine yukoje kimwili na kihali.

Kushindwa huku ndiko ambako huwafanya binadamu kuwapa wenzao kile ambacho kama wengepewa wao kungezuka balaa kubwa. Binadamu wamekuwa wakijaribu kuridhisha miili yao na pengine nafsi kama siyo tamaa zao kwa kuwafanyia wengine lile ambalo kwao lingekuwa ni gumu sana kulivumilia.

Leo hii kuna binadamu ambao kwa kujali fedha wanauza sumu kwa binadamu wenzao. Kwa kutaka fedha huuza vyakula ambavyo wanajua wazi kwamba, vitawashuru afya za wengine na kuwauwa. Wanauza vyakula hivyo wakiwa na uhakika kwamb, baada ya muda fulani, hao waliouziwa wataugua kansa au maradhi mengine hadi kufa. Lakini ni wazi wao wasingekubali kufanyiwa jambo hilo.

Kuna wale ambao kwa matumizi ya vyeo vyao huwakosesha wengine haki zao kwa sababu tu wengine hao hawana nguvu na uwezo wa kupambana nao. Hawa kwa makusudi huwafanya watu wengi kuishi katika ulitima wa kudumu wakati wangeweza kuinuka na kuishi kama wao.

Kuna kundi kubwa la binadamu ambalo kamwe halijawahi kufanya jema kwa wengine, halijawahi kutamka jema kwa wengine na halijawahi kufikiria jema kwa wengine. Kundi hili lina watu ambao wao kila siku wanafikiria ni kwa namna gani watatumia ujinga wa wengine kwa manufaa yao, ujinga wa wengine kwa kujupatia ziada na “kutanua” huku wengine hao wakiporomoka na kuingia kwenye shimo la kiza cha ukosefu na majuto.

Umefika wakati ambapo inabidi tuanze kuhushimu nguvu za maumbile, inabidi tuanze kuhushimu ubinadamu katika ujumla wake. Inabidi tujue kwamba kinachotufanya tusimame leo na kujidai, kujuvuna na kujiona tu bora sana ni kwa sababu kuna banadamu wengine wanaotuzunguka. Kinachotufanya leo hii tutamani kuonekana wakubwa zaidi, wenye uwezo zaidi na wenye heshima zaidi ni kuwepo kwa binadamu hata kidogo kama tunavyodhani, bila binadamu wengine kuwepo.

Mbaya zaidi ni kwamba, sisi siyo binadamu kamili kama wenzetu siyo kamili. Ukamilifu wao ndiyo unatupa sisi ukamilifu. Ukitaka kuthibitisha jambo hili unaweza, kwani ni rahisi sana. Hebu anza sasa kutenda yale ambayo hata wewe ungependa kutendewa na kuacha kuwatenda wengine yale ambayo hata wewe usingependa kutendwa. Tuna uhakika baada ya muda fulani utagundua ukweli fulani na bila shaka utawasiliana nasi kutufahamisha. Hutapoteza chochote kufanya jaribio hilo bila shaka.
MWISHO.......
Makala hii nimeichukua kutoka kwenye kitabu cha Maisha na Mafanikio kilichoandikwa na Hayati Munga Tehenan ambaye alikuwa ni Mwalimu mzuri wa maarifa ya Utambuzi akitoa elimu hiyo kupitia magazeti yake ya Jitambue, vitabu na semina zake nchini Tanzania kabla ya kufariki dunia.

5 comments:

chib said...

Habari nzuri, lakini umepata haki miliki ya kutoa habari hii :-)

~PakKaramu~ said...

Visiting you staf nurse

Serina said...

Dada Yasinta umenigusa sana hapa... huwa nasema kuwa binadamu ni nafsi yake... kazini huona sana madaktari wanavyowabagua wagonjwa saa zingine... ukisikia mheshimiwa fulani kafika na ambulance basi waache wagonjwa wengine wote ukamuhudumie yeye kwanza...ingawa ameteguka tu! Naamini cha muhimu ni kuheshimu kila kilicho hai.

Chacha Wambura said...

mh! Yasinta, ni kweli nawe hufanya hivo kadiri ya mfano wa Serina?....lol

ni elimu murua saaana. Usingwiii..lol

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Chib! usiwe na hofu nimepata haki miliki:-)

PakKaramu thank you.

Da Serina unafikiri uwongo ni kweli kabisa mambo hayo yapo hata sielewi kwa nini. Wakati wote tunajua binadamu wote ni sawa.

Chacha Wambura :-) mi si bagui watu kwangu wote ni sawa.usengwili na veve kwa kugendela hapa kila wakati:-)